MAMA ALIYEPORWA MTOTO ALBINO AFANYIWA UPASUAJI WA KICHWA -GEITA

Ester Jonas (30) ambaye ni mama mzazi wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati akiwa amelazwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC). 
Mama wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ambaye alitekwa juzi na watu wasiofahamika mkoani Geita, amefanyiwa upasuaji wa kichwa na jopo la madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mjini Mwanza.
Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Ester Jonas (30), alilazimika kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushambuliwa kwa kukatwa mapanga na watu hao ambao walimteka mtoto wake juzi akiwa amembeba mgongoni nyumbani kwake.
Mkuu wa Kitengo cha dharura cha Hospitali ya Bugando, Dk Darick David alisema mama huyo alifikishwa hapo jana akiwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Namkumbuka mwanangu Yohana Bahati,” hayo ni maneno aliyoyasema mama mzazi wa mtoto huyo akiwa hospitalini hapa kwenye chumba namba 903 cha uangalizi maalumu (ICU).
“Kama mnavyomuona hali yake siyo nzuri, hata kuzungumza hawezi, alikatwa panga kichwani jeraha kubwa liko puani, tumelazimika kumfanyia upasuaji wa kichwa ili kusafisha damu iliyokuwa imeganda ndani,” alisema Dk David na kuongeza: “Bado anatatizo kubwa na madaktari bingwa wanaendelea kumchunguza.”
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Profesa Alfred Mteta alisema: “Inasikitisha kuona binadamu unamfanyia unyama binadamu mwenzako, kamwe vitendo hivi haviwezi kukubalika tumempokea mgonjwa huyu na madaktari wanaendelea kumpatia matibabu ili kuokoa maisha yake.”

Mbunge Viti Maalumu
Mbunge wa Viti Maalumu anayewawakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi bungeni, Al-Shaymaa Kwegyir ametaka nguvu zinazotumiwa na polisi kuwakamata majambazi, zitumike pia kuwasaka wanaoteka na kuwaua watu wenye ulemavu huo.
Kauli ya Kwegyir imekuja baada ya kuanza kuibuka kwa matukio ya utekaji na kuwaua wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina.
Hivi karibuni, mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi mkoani Geita alitekwa na mama yake kucharangwa mapanga. Utekaji huo umetokea ikiwa ni siku 50 sasa tangu kutoroshwa kwa mtoto, Yohana mkoani Mwanza.
“Polisi wana nguvu za kukamata majambazi, kwanini nguvu hiyo isitumike kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivi, tumeanza kuwa na shaka juu ya utendaji kazi wao kuwa unaegemea upande fulani,” alisema Kwegyir.
Alisema kuna haja ya serikali na polisi kuongeza jitihada ili kumaliza tatizo hilo linaloonekana kushamiri kwa kasi.
“Nilikuwa Nyakato mwezi uliopita, kuna mtoto wa miaka minne alinusurika kunyakuliwa na watu waliokuwa kwenye pikipiki, kwa bahati nzuri mama yake alimuwahi, matukio kama haya yanaashiria kuwa hali ni mbaya,” alisema.

Barwany alia na mfumo
Akizungumzia matukio hayo, Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, alidai kutopatiwa ufumbuzi kwa tatizo hilo la utekaji na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kunaashiria kuwa wahusika wakuu wa vitendo hivyo huenda wanafahamika hivyo kuna baadhi ya watu wameamua kuwalinda.
Barwany alisema inashangaza kuona Serikali ikishindwa kulipatia uzito suala hilo kwa kuendelea kuwaacha wahusika wakiendeleza unyama wao.
“Ni jambo la aibu kwa Serikali kushindwa kuchukua hatua, tumeshapiga sana kelele mpaka inafikia hatua tumeamua kumwachia Mungu maana nguvu inapelekwa kwa waganga wa kienyeji, lakini ukweli ni kwamba kuna watu nyuma yao,” alisema Barwany na kuongeza;
“Nashangaa mambo haya yanavyoshika kasi wakati huu wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu na kama mwelekeo ndiyo huu, basi tusubiri matukio mengi zaidi ya haya.”
Alifafanua kuwa viongozi wengi wa Serikali wamekuwa wakipiga kelele pale tukio linapotokea, baada ya hapo hakuna ufuatiliaji unaoendelea.
Alisema kuthibitisha hilo, hata Bunge mara kadhaa limeshindwa kujadili suala hilo kwa madai kuwa kuna mambo mengine yenye umuhimu zaidi licha ya kutambua kuwa maisha ya walemavu hao yanazidi kuwa hatarini.
Itakumbukwa, Januari 29, 2009, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimwaga chozi bungeni mjini Dodoma kuonyesha uchungu aliokuwa nao dhidi ya mauaji ya albino yaliyokuwa yameshamiri nchini.
Alitamka wazi kuwa ‘wanaoua albino nao wauawe’.
Maalbino Geita
Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngoz (Tas) mkoani Geita, kimeyahusiha matukio ya mauji hayo na Uchaguzi Mkuu huku baadhi ya wanasiasa wakitajwa kuhusika.
Kaimu Mwenyekiti wa Tas Mkoa wa Geita, Isaack Timothy akizungumza juzi baada ya tukio la mtoto Yohana Bahati(1) kutekwa Februari 15 saa 2 usiku, alisema suala hilo ni la wazi kwa kila Mtanzania ambaye akitafakari kwa makini anaweza kubaini hivyo.
Makachero kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, wamewasili Geita kuwasaka washukiwa wa utekaji wa mtoto Yohana.
Mtoto huyo mkazi wa kijiji cha Ilelema wilayani Chato mkoani Geita, alitekwa na watu wasiojulikana wakiwa wawili ambao walivamia nyumbani kwa wazazi wake na kumjeruhi mama yake.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alithibitisha kuwasili kwa makachero hao ambao wanaungana na wa Geita kuhakikisha mtoto huyo anapatikana.
“Pia tunashirikiana vya kutosha na askari wa mikoa mingine...na wananchi tunaomba watuunge mkono, wakiona kuna mtu wanamtilia shaka labda kwa kuomba maji, au kuuliza njia watoe taarifa…kuna polisi jamii huko. Kila kata na tarafa kuna polisi washirikiane na hao askari,” alisema Konyo.
Konyo alisema familia hiyo, ilikuwa na watoto watatu wenye ulemavu wa ngozi ambao ni pamoja na Shida (11) na Tabu (3) ambao kwa sasa wanahifadhiwa na Serikali ya Wilaya ya Geita.

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII

Previous
Next Post »
Thanks for your comment